TALII NA TEMBELEA HIFADHI YA TAIFA YA SERENGETI
Serengeti (Wilayani Serengeti) mkoani Mara katika ukanda wa ziwa victoria (lake Victoria zone) mwa jamhuri ya muungano wa Tanzania
Chanzo Cha Chimbuko Halisia Kimaelezo Na Ubunifu (Mwalimu Edgardo Kabulwa Welelo
Ukweli Wa Mambo Kuhusiana Na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti (Serengeti National Park) Wilayani Serengeti Mkoani Mara Katika Ukanda Wa Ziwa Victoria (Lake Victoria Zone) Mwa Jamhuri Ya Muungano Ya Tanzania;
Hifadhi ya Taifa ya Serengeti (Serengeti National Park) kijiografia inapatikana katika Ukanda wa Ziwa Victoria (Lake Victoria Zone) Wilayani Serengeti Mkoani Mara.Ikumbukwe na ieleweke ya kwamba kihistoria toka hapo zamani ya miaka mingi sana iliyopita kabla ya ‘Watawala Wakoloni’ na vilevile kabla ya uhuru wa ‘‘TANGANYIKA’’ tarehe 9/12/1961, eneo la leo hii linalojulikana kama Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (Ngorongoro Conservation Area Authority) kabla ya kumegwa na kutenganishwa mnamo mwaka wa 1959 kutoka katika Hifadhi ya ‘’SERENGETI KUU’’(‘GREAT SERENGETI’’) kama eneo la uhifadhi linalojitegemea peke yake na pia lenye kuwa na uongozi na mamlaka yake yenyewe kama vile ilivyo kwa taasisi nyiginezo za kiserikali za uhifadhi kama vile TANAPA, TAWA na TFS, ni ya kwamba ukweli halisia wa kihistoria ni kuwa hapo zamani maeneo haya mawili kwa pamoja ‘’Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro’’(Ngorongoro Conservation Area Authority) na ‘’Hifadhi ya Taifa ya Serengeti’’(Serengeti National Park) ilikuwa ni eneo moja kubwa kwa wakati mmoja la uhifadhi ikifahamika kwa kipindi cha nyakati zile za miaka ya zamani kupita kama ‘’SERENGETI KUU’’ (‘’GREAT SERENGETI’’) pale ambapo Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ilipoanzishwa mnamo mwaka wa 1951 kama hifadhi ya kwanza na iliyo kongwe nchini na katika kipindi hicho cha mwaka wa 1951 ‘’Serengeti Kuu’’ ilipoanzishwa ni kwamba jamii ya kifugaji ya kabila la ‘‘WAMAASAI’’ ilikuwa ikiendelea ikiishi katika maeneo yote haya mawili kwa wakati mmoja sambamba na mifugo yao na wanyamapori.
Miaka 8 baadaye kupita ya uanzishwaji wake ‘’SERENGETI KUU’’ (‘GREAT SERENGETI’) mnamo mwaka wa 1951 na kufikia mnamo mwaka wa 1959 ndipo uamuzi wa kuigawanya ‘’SERENGETI KUU’’(‘GREAT SERENGETI’) katika maeneo mawili tofauti katika uhifadhi wa kimkakati ukafanyika kwa kuazishwa eneo la ‘’Hifadhi Mseto’’(Multiple Land Use Area) ambayo leo hii ikijulikana kama ‘’Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro’’(Ngorongoro Conservation Area Authority) na hatimaye ikapelekea jamii yote ya kifugaji ya kabila la ‘’WAMAASAI’’ kuhamishiwa eneo la leo hii la ‘’Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro’’ na kuondoka kabisa kutokea katika ‘’Hifadhi ya Taifa ya Serengeti’’ (Serengeti National Park) ambako pia walikuwa wakiishi ili kupisha uhifadhi wa ‘’SERENGETI’’ iwe hifadhi maalumu kimkakati kwa ajili ya uhifadhi wa wanyamapori peke yake. Kihistoria, jamii ya kifugaji ya kabila la ‘Wamaasai’ ni kwamba chimbuko na asilia yao walikotokea na pia kuaminika na wataalamu wa kihistoria ni katika Taifa linalofahamika leo hii kama Sudani Kusini (SOUTH SUDAN) na ndio jamii ya kwanza kukanyaga na kutawala ardhi ya Serengeti na Ngorongoro kabla ya jamii nyinginezo za makabila na pia jamii ya kifugaji ya kabila la ‘Wamaasai’ imeishi maeneo haya kwa miaka mingi sana iliyopita ya ‘Mababu na Mabibi’ zao sambamba na Wanyamapori katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti(Serengeti National Park) na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (Ngorongoro Conservation Area Authority). Asili ya neno au jina Serengeti limetokana na matamshi ya lugha ya Kabila la Wamaasai (‘SIRINGET’) lenye kumaanisha ‘’Uwanda Mpana’’ au ‘’Ardhi Tambarare’’ iliyotawaliwa na uoto wa asili wa mimea ya nyasi fupi na nyasi ndefu isiyokuwa na miti (Short and Long Grassy Plains) Isiyokuwa na Mwisho’
Ushauri kwa watalii raia wa tanzania katika kujiandaa na kujipanga kimaandalizi na kikamilifu kwa safari utalii
Watalii wa ndani waanze na utafiti makini unaohusiana na kukusanya maelezo na taarifa za hifadhi yenyewe kwa kupata maelezo ya gharama za wakati husika kama vile viingilio hifadhini, gharama za kupiga kambi na kadha wa kadhalika. Vyanzo vya taarifa nyinginezo ni pamoja na kupitia tovuti ya TANAPA (www.tanzaniaparks.go.tz). Vyanzo vinginevyo vya taarifa au maelezo ni pamoja na kuwasiliana na wadau wa sekta ya utalii na usafirishaji wanaotoa huduma za shughuli za utalii katika hifadhi hii ya Taifa ya Serengeti. Gharama zake zikoje au zinatofatianaje vipi? Fedha zinazohitajika na upatikanaji wake. Mwisho kabisa ni mpango mkakati wa fedha na bajeti ya matumizi yenyewe ya fedha hizo katika safari utalii ya matembezi hifadhini.
Hifadhi ya Taifa ya Serengeti (Serengeti National Park) ilianzishwa rasmi mnamo mwaka wa 1951. Ikumbukwe na ieleweke ya kwamba mwaka huo wa 1951 ilikuwa ikihusisha kwa pamoja na eneo linalofahamika leo hii kama ‘’Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro’’ (Ngorongoro Conservation Area Authority) na wakati wa kipindi hicho cha uanzishwaji wake wa mwaka wa 1951 ilifahamika kama ‘’SERENGETI KUU’’ (‘GREAT SERENGETI’) kabla ya eneo la Ngorongoro kutenganishwa na kujitegemea kutoka ‘’Serengeti’’ hapo mnamo mwaka wa 1959 ikifahamika leo hii kama ‘’Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro’’ (NGORONGORO CONSERVATION AREA AUTHORITY).
Mpaka kwa wakati huu kwa sasa ukubwa wa eneo la Hifadhi ya Taifa ya Serengeti (Serengeti National Park) ni ukubwa wa eneo la ardhi lenye kuwa na kilometa za mraba takribani 14,763 ( au sawa na maili za mraba takribani 5700). Kwa hivi sasa, ‘’Hifadhi ya Taifa ya Serengeti’’ (Serengeti National Park) ndio hifadhi ya tatu kwa ukubwa wa eneo la ardhi baada ya Hifadhi ya Taifa ya ‘‘NYERERE’’ (Zamani ikifahamika kama SELOUS GAME RESERVE), na ‘’Hifadhi ya Taifa ya Ruaha’’ (‘’Ruaha National Park’’) ipatikanayo Mkoani Iringa ambayo yenyewe ni ya pili kwa ukubwa wa eneo la ardhi nchini Tanzania.
Hifadhi ya Taifa ya Serengeti(‘’Serengeti National Park’’) inafikika kirahisi kabisa takribani umbali wa kilomita 335 (au sawa na maili 208 kwa njia ya usafiri wa barabara kutokea upande wa Magharibi ya Mji wa Arusha (Arusha City). ‘’Seronera’’ ndio yaliyo kuwa Makao Makuu ya zamani ya ‘’Hifadhi ya Taifa ya Serengeti’’ (‘’Serengeti National Park’’) na pia ndilo eneo linalopatikana katikati kabisa ya hifadhi hii na vilevile ni kitovu kikuu cha utalii hifadhini Serengeti. Ni sawa na umbali wa mwendo wa takribani saa 5 mpaka 6 kutokea Mji wa Arusha (Arusha City) katika mwendo wa kawaida.Ikumbukwe na ieleweke ya kwamba kwa hivi sasa Makao Makuu Mapya ya ‘’Hifadhi ya Taifa ya Serengeti’’ yamehamishiwa katika eneo linalojulikana kama ‘’FORT IKOMA’’ ambapo hapo zamani ilikuwa ni ‘’Ngome ya Watawala Wakoloni Wajerumani
Ni pamoja na mtawanyiko wa hapa na pale Hifadhini Serengeti wa ‘’Miamba ya Ardhini katika Uso wa Ardhi’’ (‘’Rocky Outcrops/Kopjes’’), ‘’Maeneo Wazi au Uwanda Mpana wa Ardhi Tambarare’’ wenye kutawaliwa na uoto wa asili wa mimea wa nyasi fupi na nyasi ndefu (‘’Short and Long Grassy Plains’’) katika upande wa Kusini Mwa Hifadhi ya Serengeti (‘’Southern Serengeti Plains’’) inayopakana kimipaka na ‘’Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro’’ (Ngorongoro Conservation Area Authority), ‘’Uoto wa asili wa mimea ya miti ya Migunga (Acacia/Achelia) sambamba na uoto wa asili wa mimea nyasi katika maeneo wazi ya nyika na mapori (Savanna Grassland ) katikati ya Hifadhi ya Serengeti (‘’SERONERA’’), ‘’Uoto wa asili katika Vilima’’ upatikanao katika upande wa Kaskazini mwa ‘’Hifadhi ya Serengeti’’, ‘’Mtawanyiko mkubwa’’ wa uoto wa asili wa mimea miti ya Mapori katika upande wa Magharibi mwa Hifadhi ya Serengeti, na bila kusahau ‘’Mto Grumeti (GRUMETI RIVER)’’ maarufu kwa idadi kubwa ya Mamba aina ya (Nile Crocodiles), na kadha wa kadhalika.
Hali ya hewa kutoka katika ‘’Usawa wa Bahari’’ ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti(‘’Serengeti National Park’’) ina anzia ‘’Mita 950 mpaka 1850’’. ‘’Seronera’’ eneo ambalo ni katikati kabisa ya ‘’Hifadhi ya Serengeti’’ na pia kituvo kikuu cha utalii, ndio yaliyokuwa Makao Makuu ya awali ya ‘’Hifadhi ya Taifa ya Serengeti’’ ni takribani ‘’Mita 1530’’.Kwa hivi sasa ‘’Makao Makuu ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti’’ yamehamia katika eneo linalojulikana kama ‘’FORT IKOMA’’ eneo ambalo kihistoria ilikuwa ni ‘’Ngome ya Watawala Wakoloni Wajerumani’’.
Ni pamoja na Wanyamapori jamii ya ‘’Walaji Wa Nyama’’ (Carnivores) kama vile Simba (Lions), Chui (Leopard), Fisi Madoadoa (Spotted Hyenas), Duma (Cheetah), Mbwa Mwitu (Wild dogs) na wengineo walio wengi. Vivutio vinginevyo ‘’Hifadhini Serengeti’’ ni kama vile ‘’Uhamaji Wa Wanyamapori’’ kwa msimu (Animal Migration). Mfano hai ni wanyamapori jamii ya Nyumbu (Western- White Bearded Wildebeest), Pundamilia (Common/ Plains/Burchell’s Zebra), na wanyamapori jamii ya Swala (Gazelles). ‘’Miamba ya Ardhini’’ katika uso wa Ardhi (Rocky Outcrops/Kopjes), Maeneo wazi au ‘’Uwanda wa Ardhi Tambarare’’ wenye kutawaliwa na uoto wa asili wa mimea wa nyasi fupi na ndefu (Short and Long Grassy Plains), Idadi kubwa ya viumbe hai ndege wahamaji (Migratory birds), ‘’Idadi kubwa ya Ndege Mbuni (Maasai Ostrich)’’, na kadha wa kadhalika.
Wanyamapori wapatikanao ‘’Hifadhini Serengeti’’ (Serengeti National Park) ni wengi sana na pia ni wa aina mbalimbali kama vile Mbwa Mwitu(Wild dog),Tumbili/ Ngedere (VervetMonkeys/Black – Faced Monkeys),Vicheche(Zorilla),Kuro(aina zote mbili;Common Waterbuck & Deffasa Waterbuck), Ngiri(Common Warthog), Paa(Suni), Taya(Oribi), Kindi(Squirrels), Palahala(Sable Antelope),Korongo(Roan Antelope), Tohe(Bohor Reedbuck),Pimbi(Rock Hyrax & Bush Hyrax),Viboko(Common Hippopotamus/ East Africa Hippopotamus),Swala Tomi(Thomson Gazelles), Kongoni (Coke’s Hartebeest),Nguchiro wa aina mbalimbali (Mongooses Races),Nyumbu (Western – White Bearded Wildebeest),Nyegere(Ratel/HoneyBadger), Digidigi(Kirk’sDikDik),Pongo/Mbawala(Bushbucks),Isha(Steenbok/Steenbuck), Pofu(Patterson Eland/East African Eland),Mhanga(Aardvark/Ant- Bear), Nyani(Olive Baboon/Savanna Baboon), Nguruwe Mwitu(Bush Pig),Mbweha Masikio(Bat – Eared Fox),Mbogo/Nyati(African/Savanna/CapeBuffalo),Chui(Leopards), Simba(Lions),SwalaPala(Impala),SwalaGranti(GrantGazelle), Twiga(Kilimanjaro/MaasaiGiraffes),Tembo/Ndovu(African/Bush/Savanna Elephant),Faru(Black Rhinos),Mbega wenye kuwa na rangi nyeusi na nyeupe (Black and White Colobus Monkeys),Fungo(African Civet),Kanu(Common Genet), Swala Twiga (Gerenuk),aina zote 3 za Mbweha(JACKALS) kama vile Bweha Dhahabu (Common/Golden Jackal),Bweha Mgongo Mweusi(Black – Backed Jackal),pamoja na Bweha Mstari Mbavuni(Side – Striped Jackal), Mbuzi Mawe (Klipspringers), Tandala Mdogo(Lesser Kudu),Tandala Mkubwa(Greater Kudu),Choroa(Fringe – Eared Oryx), Mondo(Serval Cat),Nyamera (Topi),Funo/Ngarombwi(Common/Bush/Gray Duiker) na wengineo walio wengi. Ikumbukwe na ieleweke ya kwamba kitafiti na kisayansi ‘’Hifadhi ya Taifa ya Serengeti’’ (Serengeti National Park) imerekodiwa na kuripotiwa kuwa na takribani zaidi ya spishi 500 za viumbe hai ndege. Miongoni mwa wachache katika orodha hiyo ya spishi zaidi ya 500 ni pamoja na ‘’Ndege Wawindaji na Walaji wa Nyama’’ (Birds of Prey/Raptors) takribani spishi 34 kuweza kurekodiwa na kuripotiwa kama vile; Tumbusi Kichwa Kikubwa (Lappet – Faced Vulture), Tumbusi Mgongo Mweupe (African White – Backed Vulture), Tumbusi Mdogo (Hooded Vulture), Tumbusi Mbuga (Ruppell’s Vulture), Tumbusi Mweupe (Egyptian Vulture) pamoja na Ndege Karani/Kilemba (Secretary Bird). Wengineo ni kama vile Ndege Mbuni (Maasai Ostrich), Tandawala Mkubwa (Kori Bustard), Taji/Korongo - Taji (Grey Crowned Crane), Kanga (Helmeted Guinea Fowl), Mwezi Maridadi (Superb Starling), ‘’Mwezi Jangwa’’ (Hildebrandt’s Starling), ‘’YangeYange’’ (Cattle Egret), na kadha wa kadhalika.
‘’Hifadhi ya Taifa ya Serengeti’’(Serengeti National Park) ina angukia katika ‘’Maeneo ya Uoto wa Asili wa Maeneo Makame’’ katika ukanda unaofahamika kitaalamu kama ‘’(Somali – Maasai Region)’’ ambapo uoto wa asili wa mimea asilia ya miti ya Migunga (Acacia/Achelia) na Mbabara au Mturituri (Commiphora) umetawala na kutalamaki.Katika ukanda wa eneo hili mvua kwa mwaka kawaida ni chache sana takribani ‘’Milimita 300 mpaka 700’’.Vilevile kuna ‘Maeneo wazi ya Ardhi Tambarare’’ yenye kuwa na uoto wa nyasi fupi na ndefu (Short and Long Grassy Plains) katika upande wa Kusini mwa Hifadhi ya Serengeti(Southern Serengeti Plains). Vilevile Uoto wa Asili wa Msitu unaostawi kufuata Mkondo wa Mto (Gallery/Riverine Vegetation).Kwa ujumla wake ‘’Hifadhi ya Taifa ya Serengeti’’ (Serengeti National Park) ina aina ‘’7 za Uoto wa Asili wa Makazi’’, kama ifuatavyo katika orodha hii hapa kwa chini yake;
- Uoto wa Asili wa Makazi ya Misitu (FOREST);
Uoto huu wa asili hupatikana kwa kiwango kidogo ‘’Hifadhini Serengeti’’ hususani katika maeneo ya kandokando ya mito na chemichemi za maji sambamba na ‘’Uoto wa Asili wa Msitu Unaostawi Kufuata Uelekeo wa Mikondo ya Mito’’ (‘’Gallery/Riverine Forest’’).
- Uoto wa Asili wa Mimea wa Miti ya Mapori (WOODLAND).
Ni aina ya uoto wa asili wa mimea ya miti yenye kuwa na tabia ya kupukutisha majani yake ya juu katika matawi ya miti (Deciduous) kwa ajili ya kujihifadhia maji wakati wa kipindi cha msimu wa kiangazi.Mifano hai ya jamii za mimea ya miti ni pamoja na (Koo za mimea ya miti kama vile ‘Combretum’, ‘Terminalia’, ‘Acacia/Achelia’ pamoja na ‘Commiphora’.
- Uoto wa Asili wa Mimea Nyasi mchanganyiko na Miti ya Vichaka (WOODED GRASSLAND);
Uoto huu wa asili hutawaliwa na mimea ya miti yenye kutawaliwa na miba (Thorns) sambamba na uoto wa mimea ya nyasi.Mfano hai ni miti ya Mjunju (Desert Date) ambayo hupendelea kustawi zaidi katika maeneo yenye kuwa na ardhi kame nyeusi (Black cotton clay soil).
- Uoto wa Asili wa Mimea Miti ya Mapori Halisia (BUSHLAND);
Uoto huu wa asili wa mimea ya miti unahusisha miti ambayo ni kijani kibichi kupitia majani yake ya juu kukaa mda mrefu (Evergreen) mpaka mimea ya miti ambayo kitabia nayo pia hupukutisha majani yake ya juu katika matawi ya miti kwa kiwango cha wastani (Semi – deciduous).Mtawanyiko wa aina hii ya uoto wa asili hupatikana katika baadhi ya maeneo ya ‘’Kaskazini mwa Hifadhi ya Serengeti’’.Vilevile aina hii ya uoto wa asili huweza kuonekana katika vichuguu vya mchwa (Termite Mounds) katika upande wa Magharibi mwa Hifadhi ya Serengeti.’’Koo za miti ya Migunga (Acacia/Achelia) imetawala’’.
- Uoto wa Asili wa Mimea ya Nyasi na Mapori Mchanganyiko (BUSHED GRASSLAND);
Hili ni eneo la ardhi Hifadhini Serengeti ambapo uoto wa asili wa mimea ya nyasi pamoja na miti ya mapori imechanganyikana kwa pamoja (Bushed Grassland).Eneo hili la uoto wa asili wa mimea umetawaliwa na mimea ya miti ya ‘’Koo ya miti ya Migunga(Acacia/Achelia)’’na ‘’Koo ya miti ya Mbabara au Mturituri(Commiphora)’’.
- Uoto wa Asili wa Mimea upatikanao katika ‘’Mimba ya Ardhini katika Uso wa Ardhi (Rocky Outcrops/Kopjes);
Huu ni uoto wa asili wa mimea maalumu katika ‘’Miamba ya Ardhini katika uso wa Ardhi’’ (Kopjes/Rocky Outcrops) ambapo hupatikana aina mbalimbali za uoto wa asili wa nyasi sambamba na miti mifupi na mirefu.
- Uoto wa Asili wa Mimea Nyasi fupi na ndefu (GRASSLAND/SHORT&LONG GRASSY PLAINS) katika ‘’Ardhi Tambarare iliyofunikwa na Tabaka la Miamba ya Volkano Kiasili’’ katika upande wa kusini mwa Serengeti (Southern Serengeti Plains);
Kiasili eneo hili la uoto wa asili wa mimea nyasi fupi na ndefu katika ardhi tambarare (Grassland/Short and Long Grassy Plains) linapatikana kijiografia katika upande wa kusini mwa ‘’Hifadhi ya Serengeti’’(Southern Serengeti Plains) eneo ambalo kitaalamu miti kawaida haioti na kustawi kwa wingi na badala yake eneo hili kuweza kutawaliwa na nyasi fupi na ndefu (short and long grassy plains) kutokana na eneo hili kufunikwa na tabaka la miamba ya VOLKANO ambayo kimsingi chimbuko lake na asili yake ni kutokea Milima ya Volkano ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro ( Ngorongoro Conservation Area Authority) iliyolipuka na kusambaa na kutawanyika Serengeti Kusini ya leo hii takribani (Miaka Millioni 3 Mpaka 4 iliyopita).
Mwezi wa Desemba mpaka Mwezi Julai kwa ajili ya kujionea na kushuhudia ‘’Msafara wa Uhamaji wa Wanyamapori’’ kama vile Nyumbu na Wanyamapori wengineo walio wengi. Vilevile Mwezi wa Juni mpaka Mwezi Oktaba kwa ajili ya kujionea ‘’Wanyamapori Wawindaji na Walao Nyama (Predators)’’ kama vile Simba (Lions), Chui (Leopards), Fisi Madoadoa (Spotted Hyenas), Duma (Cheetah) na wengineo walio wengi.
Mambo yaliyo ya muhimu ya kujiuliza katika safari utalii yenu ya matembezi hifadhini, je mtajibebea vyakula vyenu wenyewe vya kujipikia? Au hakuna ulazima huo na badala yake mtapata huduma hiyo katika sehemu ambazo huduma ya chakula inapatikana.
Kama mtalala ndani ya hifadhi, je mtapiga kambi na katika kupiga kambi ni lazima mbebe mahema yenu wenyewe au mtakodisha? Ikumbukwe na ieleweke ya kwamba kunapatikana huduma kadhaa za huduma ya malazi au kulala Hifadhini Serengeti. Hoteli za kitalii za SERONERA na LOBO ni mojawapo ya HOTELI KONGWE ambazo kihistoria zilianzishwa miaka ya zamani ya 1970. Hoteli ya kitalii ya Seronera (Seronera Wildlife Lodge) inapatikana katikati kabisa ya Hifadhi ya Taifa Serengeti takribani umbali wa kilomita 145 kutokea Bonde la Ngorongoro (Ngorongoro Crater) katika ‘’Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro’’ (Ngorongoro Conservation Area Authority) na vilevile ni sawa na umbali wa takribani kilomita 335 kutokea Mji wa Arusha (Arusha City). Hoteli hii ya Seronera ina vitanda vya kulaza wageni watalii takribani 75. Kwa upande mwingine Hoteli ya LOBO (Lobo Wildlife Lodge) yenyewe inapatikana upande wa ‘’Kaskazini mwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti’’ karibu kabisa mpakani na Taifa la Kenya na Tanzania. Kama unatokea eneo la SERONERA ambapo ndio katikati kabisa mwa ‘’Hifadhi ya Serengeti’’ kuelekea LOBO ni sawa na mwendo wa takribani saa moja na nasu katika mwendo wa uendeshaji gari wa kawaida na vilevile inachukua takribani kilomita 80 kuweza kufika LOBO. Hoteli hii ya LOBO imejengwa katika Mwamba Mkubwa wa Ardhini katika uso wa ardhi (Rocky Outcrops/Kopjes) ambapo hutoa fursa nzuri ya mandhari na muonekano mzuri wenye kuvutia na kupendeza wa ‘’Ardhi Tambarare’’ ya uoto wa asili wa mimea ya nyasi fupi na ndefu za ‘’Serengeti Kusini’’ (Short and Long Grassy Plains of Southern Serengeti Plains). Hoteli ya LOBO nayo pia ina vitanda takribani 75 vya kulaza wageni watalii inayokaribiana kwa ukaribu kama jinsi ilivyo katika Hoteli ya SERONERA. Neno au jina ‘LOBO’ ni neno asilia la jamii ya kabila la ‘Wamaasai’ ikimaanisha ‘eneo au sehemu inayomilikiwa na mtu mmoja’. LOBO hujipatia chanzo cha maji yake kutokea chemichemi za maji za LOBO takribani kilometa tatu kutokea LOBO. Hoteli nyinginezo za kitalii ‘’Hifadhini Serengeti’’ ambazo hutoa huduma ya malazi na pia chakula ni kama vile SOPA LODGE (ina vitanda vya kulaza wageni watalii takribani 160), SERENA LODGE (ina vitanda vya kulaza wageni watalii takribani 144), HUKA LODGE (ina vitanda vya kulaza wageni watalii takribani 80), GRUMETI RIVER CAMP (ina vitanda vya kulaza wageni watalii takribani 20), na MIGRATION CAMP (ina vitanda vya kulaza wageni watalii takribani 42). Kilicho cha muhimu kuliko vyote ni kwamba ‘’Hifadhi ya Taifa ya Serengeti’’ ina maeneo mengi ya kutosheleza na kukidhi mahitaji ya wageni watalii wa ndani na nje ya kupiga kambi za jumuiya (Public Campsites) na kambi maalumu (Special Campsites) pamoja na HOSTELI.
Umakini mkubwa katika eneo hili ni la umuhimu kwa wahusika ambao ndio waandaaji wa safari utalii ya matembezi hifadhini kupewa kipaumbele cha hali ya juu. Mambo muhimu ya maandalizi ya usafiri, vibali vya viingilio, huduma za chakula, malazi au kulala na mengineyo yaliyo mengi. Haya yote ndio yatakayokamilisha safari utalii ya matembezi hifadhini. Je, safari utalii yenu ya matembezi hifadhini inaendeka au haiendeki? Jibu litapatikana baada ya utekelezaji wa mambo muhimu kukamilka.
Dharura na matatizo mbalimbali wakati mwingine huweza kujitokeza pasipo kutarajia katika safari utalii ya matembezi hifadhini. Ni vema na busara kuwa na utamaduni wa kupeana mafunzo yanayohusiana na huduma ya kwanza na namna vifaa hivyo vinavyotumika. Mwisho kabisa fedha ya tahadhari kutengwa pembeni pale ambapo chombo cha usafiri kimeshindwa kuendelea na safari utalii.
Mambo muhimu ya kufanya na kuzingatia
(kanuni na taratibu ndani ya hifadhi)
Mawasiliano ni ya muhimu na ni lazima yawepo kati yenu na hifadhi ya Taifa ya Serengeti au Makao Makuu ya Shirika la Hifadhi za Taifa, Mjini ARUSHA. Je, kipindi ambacho mtatembelea hifadhi hii ni kipindi cha wageni wengi au wageni wachache? Je mnaweza kupata sehemu ya kupiga kambi au kulala hosteli? Hili ni suala muhimu la kujiandaa na kujipanga. Kilicho cha muhimu ni kuzingatia na kuzitekeleza kwa vitendo sheria za uhifadhi wa mazingira kwa ujumla wake na sheria nyinginezo zinazotakiwa kufuatwa ndani ya hifadhi ili kuepuka faini na adhabu ambazo si za msingi na ulazima.
Vifaa muhimu vya kuchukua katika safari utalii hifadhini
Vifaa vyote muhimu katika safari utalii yenu ya matembezi hifadhini. Mfano hai ni kama vile mahema (tents) kama mtalala ndani ya hifadhi, vyombo vyenu wenyewe vya kujipika na maji ya kunywa. Orodha ni ndefu na inategemea na mtakavyojipanga kwa mujibu wa bajeti yenu kifedha wenyewe ndugu watanzania.
Huduma za mahitaji mengineyo
Ni mambo ya ziada ya mahitaji yanayojitokeza na upatikanaji wake katika sehemu husika mlipo.
Maelezo ya huduma za habari utalii wa ndani.
Kampuni ya Uelimishaji,Uratibu,Uandaaji,Uhamasishaji, na Uwezeshaji Utalii wa Ndani
Follow us:
MAWASILIANO MENGINEYO MAKAO MAKUU (TANAPA)
- Juma tatu - Ijumaa
- 8:00 Asubuhi - 4:30 Jioni
+255 272508216
info@domestictourismsafaris.c info@domestictourismsafaris.co.tz



