TALII NA TEMBELEA HIFADHI YA TAIFA KATAVI
Mkoani katavi katika nyanda za juu kusini (southern highlands) mwa jamhuri wa muungano wa Tanzania
Chanzo Cha Chimbuko Halisia Kimaelezo Na Ubunifu (Mwalimu Edgardo Kabulwa Welelo)
Ukweli Wa Mambo Kuhusiana Na Hifadhi Halisia Ya Kiafrika Ya Taifa Katavi - Mkoani Katavi (Nyanda Za Juu Kusini/ Southern Highlands); Hifadhi ya Taifa ya Katavi ipatikanayo kijiografia Mkoani Katavi kimsingi mipaka yake inapatikana katika Wilaya tatu (3) ambazo ni pamoja na Wilaya ya Mpanda, Tanganyika na Mlele. Makao makuu ya Hifadhi ya Taifa ya Katavi yapo katika eneo la SITALIKE takribani umbali wa kilometa 38 kutoka makao makuu ya Mkoa wa Katavi. Katavi, ndio yaliyo makao makuu ya Mkoa mpya uliogawanyishwa kutoka Mkoa wa Rukwa kama jinsi ilivyokuwa ikijulikana hapo zamani. Hifadhi ya Taifa Katavi inapatikana karibu kabisa na Ziwa Tanganyika. Hifadhi hii ni maarufu nchini Tanzania na barani Afrika kutokana na upatikananaji wa idadi kubwa wa aina mbalimbali za wanyamapori tangu mnamo wa miaka ya 1911 wakati wa nyakati za kipindi za utawala wa wakoloni wajerumani ikijulikana kama ‘BISMARK HUNTING GROUND’. Mnamo mwaka wa 1957 hifadhi hii ilitangazwa kuwa Pori la Akiba la Wanyamapori (Game Reserve) ikiwa na ukubwa wa kilometa za mraba takribani 2,253. Baadaye mwaka 1974 eneo hili lilipandishwa hadhi na kuwa rasmi kama Hifadhi ya Taifa Katavi. Mnamo mwaka wa 1997 Hifadhi ya Taifa Katavi iliongezewa eneo na hatimaye kufikia kilometa za mraba 4,471. Jina la hifadhi hii ya Katavi limetokana na mzimu wa kabila la Wabende aliyejulikana kama “KATABI”. Hifadhi hii inapatikana kimipaka na maeneo ya mapori ya akiba ya wanyamapori ya Rukwa kwa upande wa 72 - Mashariki, Kaskazini mwa barabara ya Sitalike Inyonga na Magharibi ya mto “KAVUU”.
Ushauri kwa watalii raia wa Tanzania katika kujiandaa na kujipanga kimaandalizi na kikamilifu kwa safari utalii
Rasilimali Fedha itafutwe na iandaliwe kwa umakini mkubwa kimatumizi na kiuhitaji katika safari utalii yenu ya matembezi na kutalii hifadhini.
Hifadhi ya Taifa ya Katavi ilianzishwa mnamo mwaka wa 1974. Hifadhi hii ya Taifa Katavi inapatikana kwa njia ya usafiri wa barabara takribani kilometa 40 Kusini Mashariki mwa mji wa Mpanda, ambayo ni makao makuu ya Mkoa mpya wa Katavi uliomegwa kutoka Mkoa wa Rukwa.
Ukubwa wa eneo la Hifadhi hii ya Taifa Katavi ni kilometa za mraba 4,471.
Hifadhi ya Taifa Katavi inafikika kwa njia ya usafiri wa barabara kiasi cha umbali wa Kilometa 40 kutoka katika Mji wa Mpanda. Ni sawa na saa 1 katika uendeshaji wa gari wa mwendo wa kawaida. Vile vile hifadhi hii inaweza kufikika kwa kutumia njia ya barabara ya Kigoma na Mbeya inayopitia Katavi. Hifadhi ya Taifa Katavi inafikika takribani mwaka mzima kwa kutumia usafiri wa gari aina ya (Four Wheel Drive) katika miezi ya Oktoba na Desemba pia kwa aina mbalimbali vya vyombo vya usafiri. Namna ya ufikaji ni pamoja na njia ya usafiri wa barabara (kutokea jijini Dares – Salaam – Mpanda kupitia Mbeya – Sumbawanga); kutokea jijini Dares – Salaam – Mpanda kupitia Tabora – Inyonga); kutokea jijini Mwanza – Mpanda kupitia Tabora – Inyonga); kutokea jijini Arusha – Mpanda kupitia Tabora – Inyonga); na vilevile kutokea Mkoani Kigoma – Mpanda kupitia Mwese – Sitalike. Kwa usafiri wa garimoshi(treni) kutokea jijini Dares – Salaam, Mwanza au Mkoani Kigoma hadi Mpanda kwa kupitia Mkoani Tabora ambapo Mpanda usafiri wa gari utakufikisha Hifadhini Katavi. Kwa kutumia ndege ndogo za kukodisha (chartered planes) ambazo hufanya safari zake za anga kutokea miji mikubwa kama vile Arusha, Dar - es – Salaam, Kigoma pamoja na Mwanza na kutua katika uwanja wa ndege wa Ikuu, Sitalike na Mpanda katika kupeleka wageni watalii katika maeneo hayo hufanya safari zake kila siku za Jumatatu na Alhamisi kupitia kampuni za ndege kama vile, ZANITAS, SAFARI AIR LINK (SAL) na COASTAL AIR.
Maziwa, mito, maeneo yenye ardhi oevu, maporomoko ya maji, sura ya eneo lenye mandhari nzuri yenye kuvutia, kuta za bonde la ufa la mlele, uoto wa asili wa mimea ya miti ya Miombo. Kijumla uoto wa asili unaovutia kwa uwepo wa misitu iliyofunga mpaka misitu ya wazi, vichaka, uwanda wa nyasi, maziwa ya msimu na maziwa ya kudumu, mabwawa pamoja na uoto wa asili kandokando za mito huifanya Hifadhi kuwa na mvuto wa kipekee. Hifadhi ya Taifa Katavi pia ina aina nyingi za maua wakati wa kipindi cha mvua za masika, aina mbalimbali za mimea miti na majani. Kisayansi na kitafiti aina za mimea miti takribani 226 zimekwishatambulika zikiwemo aina 3 zenye kuwa na mvuto wa kipekee kisayansi. Uhai wa Hifadhi ya Taifa Katavi unategemea zaidi mto KATUMA ambao kimsingi hutiririsha maji yake katika ziwa Katavi lenye kuwa na ukubwa wa kilometa za mraba takribani 100 mpaka 150 ikitegemeana na uwepo wa maji. Katika upande wa Kaskazini, mbuga za Chada na Katisunga zenye kuwa na eneo la kilometa za mraba takribani 425 ambazo hutuamisha maji (Flood Plain) wakati wa kipindi cha mvua za masika katikati ya Hifadhi.
Inaanzia mita 900 kutoka usawa wa Bahari. Hifadhi ya Taifa Katavi ina misimu miwili ya mvua ambayo ni mwezi wa Oktoba mpaka mwezi wa Novemba ambao ni msimu mfupi, na mwezi wa Desemba mpaka mwezi wa Mei ambao ni msimu mrefu. Wastani wa mvua kwa mwaka ni takribani milimita 950. Mwezi wa Oktoba ni kipindi ambacho Hifadhi ya Taifa Katavi inakuwa na joto la hali ya juu takribani kufikia nyuzi joto 30, na kipindi cha mwezi wa Juni ni kipindi ambacho Hifadhi inakuwa na joto la wastani na kufikia nyuzi joto 24.
- Makundi makubwa ya mammalia viboko pamoja na viumbe hai wanaotambaa (reptiles) kama vile mamba katika kuta za mto Katuma wapatikanao katika eneo la Ikuu.
- Mti wa kuzimu wa ‘Katabi’ na vilima vya mkewe ‘Wamweru’.
- Viumbe hai ndege wa aina mbalimbali wa makazi ya majini pamoja na ndege wahamao kutoka ardhi oevu ya ziwa Katavi, Katsunga, na mito Katuma na Kapapa.
- Mandhari nzuri yenye kupendeza ya ziwa Katavi pamoja na miinuko ya kichanga (sandbridge) ya Lyandi.
- Maziwa ya Katavi na Chada yanayounganishwa kwa pamoja na mto Katuma, mandhari nzuri ya eneo lenye sura ya kuvutia, maporomoko ya maji ya Chorangwa na Ndido katika mto Rungwa na Lukima kwenye mto Lukima pamoja na uoto wa asili wa Miombo unaofahamika kiutaalam (Zambezian Vegetation Region).
- Bonde la Ufa la Rukwa, Lyamba Lya Mfipa katika upande wa Magharibi pamoja na Mlele katika upande wa Mashariki. Vivutio vya utalii vipatikanavyo nje ya Hifadhi ya Taifa Katavi ni
kama vile ziwa Tanganyika, maporomoko ya maji ya Kalembo, chemichemi ya maji moto iliyopo maji moto, ziwa Rukwa na mapori ya akiba ya Rukwa na Lwafi.
- Utalii wa utazamaji wanyamapori ndani ya vyombo maalum vya utalii (safari vehicles).
- Utalii wa matembezi ya miguu chini ya usimamizi wa askari wa wanyamapori (walking safaris).
- Utazamaji wa viumbe hai ndege (Bird watching).
- Utalii wa kupiga kambi ndani ya Hifadhi (Camping site).
- Utalii wa utengenezaji Filamu.
- Utalii wa utazamaji wanyamapori wakati wa usiku (Night Game Drive).
- Utalii wa kiutamaduni (Cultural tourism)
Makundi makubwa ya Wanyamapori Mbogo au Nyati, Pundamilia, Viboko, Kuro, Swala pala na Korongo, Tembo au Ndovu, Palahala, Kongoni, Tohe, Nyamera, Ngiri pamoja na Puku. Hifadhi ya Taifa Katavi ina takribani spishi 400 za aina mbalimbali za ndege kuweza kutambuliwa kama vile, The African skimmer, Carmine bee – eater, Racket tailed roller, Miombo bush warbler, Collared palm thrush, Palm nut Vulture na kadha wa kadhalika.
Hifadhi hii ya Taifa Katavi imetawaliwa na uoto wa asili wa mimea ya miti ya Miombo kama jinsi ilivyo kijiografia katika maeneo mengi ya Kusini na Magharibi mwa Tanzania (Miombo Woodland).
Ni kuanzia mwezi wa Mei (Tano) mpaka Oktoba (mwezi wa kumi).
Inashauriwa na kupendekezwa kwa Watanzania watalii wa ndani kujibebea vyakula vyao wenyewe vya kujipikia pamoja na maandalizi mengineyo muhimu matembezini katika hifadhi. Malazi na chakula nje ya Hifadhi ya Taifa Katavi ni pamoja na nyumba za kulala wageni (Guest houses), migahawa inayopatikana katika Kijiji cha Sitalike, sehemu za huduma za vinywaji na masoko vipatikanavyo katika mji wa Mpanda umbali wa takribani kilometa 38 kutokea makao makuu ya Hifadhi ya Taifa Katavi.
Ikumbukwe na ieleweke ya kwamba kwa Watanzania watalii wa ndani watembeleao na kutalii hifadhini wanashauriwa na kusisitizwa wakajibebea vifaa vyao wenyewe vya kupigia kambi kama vile Mahema kama kipaumbele cha kwanza na kilicho muhimu kama ratiba yao ya safari utalii inahusu kulala ndani ya Hifadhi sambamba kabisa na vyakula vyao vya kujipikia pale inapobidi. Hifadhi ya Taifa ya Katavi ina malazi yanayomilikiwa na kuendeshwa na Hifadhi yenyewe na vilevile yanayomilikiwa na kuendeshwa na watu binafsi kama wawekezaji. Malazi yanayoendeshwa na kumilikiwa chini ya usimamizi wa Hifadhi ya Taifa Katavi ni pamoja na (Nyumba ya kupumzikia wageni watalii yenye kuwa na jumla ya vitanda vitano, mabanda 7 ya kulala wageni watalii yenye kuwa na jumla ya vitanda 14, na kambi za kulala wageni watalii za aina ya kambi za jumuiya (public campsites) ambazo ni mbili, na kambi maalum (special campsites) ambazo nazo ni mbili) ndani ya Hifadhi. Malazi yanayomilikiwa na kuendeshwa chini ya usimamizi wa watu binafsi kama wawekezaji ni kama vile (Kambi ya mahema ya Chada inayopatikana katika ziwa Chada, kambi ya mahema ya Katuma inayopatikana kando ya Mbuga ya Katsunga, kambi ya mahema ya wanyamapori Katavi inayopatikana kando ya Mto Ikuu, pamoja na kambi ya msimu ya Flycatcher). Malazi na chakula nje ya Hifadhi ya Taifa ya Katavi ni pamoja na nyumba za kulala wageni (Guest houses), migahawa inayopatikana katika Kijiji cha Sitalike, Hoteli, sehemu za vinywaji na masoko yanayopatikana katika mji wa Mpanda takribani umbali wa kilometa 38 kutokea makao makuu ya Hifadhi ya Taifa Katavi.
Ni pamoja na yale mambo muhimu kukamilishwa yanayofanikisha safari utalii ya matembezi hifadhini kufanyiwa kazi kwa umakini mkubwa. Tozo hizi mbalimbali ni kama vile;
1. Tozo ya uhifadhi kwa mtu mmoja katika saa 24 (miaka 16 na zaidi, miaka 5 mpaka 16, na miaka chini ya 5).
2. Tozo za kambi za jumuiya (public campsites) – miaka 16 na zaidi, miaka kati ya 5 hadi 16, pamoja na miaka chini ya 5).
3. Tozo za kambi maalum (special campsites) – miaka 16 na zaidi, miaka kati ya 5 mpaka 16, na miaka chini ya 5).
4. Tozo za malazi ya Bandas na Nyumba za kupumzikia wageni (miaka 16 na kuendelea, miaka baina ya 5 hadi 16, na miaka chini ya 5).
5. Tozo za waongozaji wageni watalii (safari guides) pamoja na huduma ya askari wa wanyamapori mwenye silaha kwa kundi la watalii.
6. Tozo za kambi za kuhamahama (Fly camping).
7. Tozo za upigaji picha za kibiashara.
8. Tozo za utalii wa matembezi ya utalii wa miguu Hifadhini (walking safaris) – matembezi ya miguu ya muda mfupi takribani saa 4 kwa watu wazima, matembezi ya miguu ya muda mfupi kwa watoto wenye umri unaoanzia miaka 12 na kuendelea, matembezi ya miguu ya muda mrefu takribani saa 4 na kuendelea kwa watu wazima, na vilevile matembezi ya miguu ya muda mrefu kwa watoto wa umri wa miaka 12 na zaidi). 76
-
9. Tozo za magari yenye kuwa na usajiri wa Afrika Mashariki (uzito usiopungua kilogramu 2000, uzito kati ya kilogramu 2001 mpaka 3000, uzito kati ya kilogramu 3001 mpaka 7000, na uzito kati ya kilogramu 7001 na kuendelea. Magari ya wazi yatalipiwa ada ya kawaida na nyongeza ya asilimia 50. Faini kwa magari aina zote yatakayosababisha ajali hifadhini na faini ya mwendo kasi pia hutozwa.
10. Tozo za utalii wa usiku (Night Game Drive) kwa watu wazima.
11. Tozo za kutua ndege za kigeni na kibnafsi (kuanzia watu 4, 5 mpaka 12, na zaidi ya watu 13). 12. Tozo za kutua ndege za Nyumbani Tanzania (kuanzia watu 4, kati ya 5 hadi 12, kati ya watu 13 hadi 20, na vilevile zaidi ya watu 20). Ikumbukwe na ieleweke ya kwamba tozo zote ni kwa ajili ya kuingia mara moja tu na kwa saa 24. Mwenye kuwa na kibali maalumu cha Mkurugenzi mkuu hapaswi kuambatana na wageni wengine. Tozo zikishalipwa hazirudishwi. Mali
Mambo muhimu ya kufahamu na kujiuliza katika safari utalii yeyote ile ya matembezi yenu hifadhini ni pamoja na kufahamu idadi kadhaa za siku zitakazohitajika au kutumika katika safari utalii yenu ya matembezi hifadhini. Hii ndio dira ya jumla jinsi safari ya matembezi hifadhini itakavyokuwa ni nini kifanyike au kirekebishwe.
Mambo muhimu ya kufanya na kuzingatia
(kanuni na taratibu ndani ya hifadhi)
Elimu itolewe kwa Watanzania watalii wa ndani waliopo katika msafara wa matembezi na utalii hifadhini kuhusiana na masuala ya huduma ya kwanza, usalama wao binafsi wenyewe hifadhini na mambo mengineyo muhimu kama vile;
1. Ni marufuku kabisa kwa wageni watalii kuingia ndani ya Hifadhi wakiwa na silaha ya aina yeyote ile.
2. Ni marufuku kabisa kwa wageni watalii kutoka nje ya magari yao isipokuwa tu katika maeneo yaliyoruhusiwa kisheria kwa ajili ya usalama wao wenyewe.
3. Ni marufuku kabisa kwa wageni watalii kutupa takataka hovyo, vichungi vya sigara au njiti za kiberiti ndani ya Hifadhi na inashauriwa na kusisitizwa kwa wageni watalii kutoka nje ya Hifadhi na takataka zao zote walizokujanazo.
4. Ni marufuku kabisa kusababisha mioto ndani ya Hifadhi.
5. Ni marufuku kabisa kwa wageni watalii kuingia ndani ya Hifadhi na Wanyama wafugwao majumbani na binadamu kama vile mbwa na paka.
6. Ni marufuku kabisa kwa wageni watalii wanapokuwa ndani ya Hifadhi kung’oa au kuchuma majani, au kufanya kitendo cha kukata na kuharibu mimea.
7. Ni marufuku kabisa kwa wageni watalii ndani ya Hifadhi kuleta au kusababisha kelele kama kupiga honi, muziki kwa sauti kubwa au aina yeyote ile ya bugudha na usumbufu kwa wageni watalii wengine.
8. Ni marufuku kabisa kwa wageni watalii wanapokuwa ndani ya Hifadhi kuwalisha wanyamapori na ndege.
9. Ni kinyume cha sheria na taratibu kuendesha chombo cha usafiri nje ya barabara maalum kwa shughuli za kiutalii au sehemu ambazo haziruhusiwi.
10. Ni kinyume cha sheria na taratibu kuendesha mwendo wa kasi chombo chako cha usafiri zaidi ya kilometa 50 kwa saa nyakati za mchana na kilometa 30 kwa saa nyakati za usiku. Ikumbukwe na ieleweke ya kwamba kuwepo ndani ya Hifadhi inaruhusiwa kuanzia saa kumi na mbili asubuhi na kutoka nje ya Hifadhi saa kumi na mbili jioni, isipokuwa tu kwenye maeneo ya kupiga kambi na kulala wageni kwa mujibu cha kibali cha watalii husika.
Vifaa muhimu vya kuchukua katika safari utalii hifadhini
Vifaa vyote muhimu vinavyohitajika katika safari ya utalii na matembezi yenu hifadhini. Kwa mfano, nguo, sabuni, dawa za meno, vifaa binafsi vya huduma ya kwanza, kamera, vitabu vya mazingira, viona mbali na vinginevyo muhimu vinavyohitajika katika safari ya kimatembezi hifadhini.
Huduma za mahitaji mengineyo
Mambo ya ziada ya mahitaji yanayojitokeza na upatikanaji wake katika sehemu husika ambapo watanzania watalii wa ndani walipo.
Maelezo ya huduma za habari utalii wa ndani.
Kampuni ya Uelimishaji,Uratibu,Uandaaji,Uhamasishaji, na Uwezeshaji Utalii wa Ndani
Follow us:
MAWASILIANO MENGINEYO MAKAO MAKUU (TANAPA)
- Juma tatu - Ijumaa
- 8:00 Asubuhi - 4:30 Jioni
+255 272508216
info@domestictourismsafaris.c info@domestictourismsafaris.co.tz



