TALII NA TEMBELEA HIFADHI YA TAIFA MKOMAZI

Mkoani Kilimanjaro na Tanga katika ukanda wa kaskazini mwa jamhuri ya muungano wa Tanzania

Chanzo Cha Chimbuko Halisia Kimaelezo Na Ubunifu (Mwalimu Edgardo Kabulwa Welelo)

Ukweli Wa Mambo Kuhusiana Na Hifadhi Ya Taifa Mkomazi (Kilimanjaro & Tanga) Pamoja Na Historia Yake; Yapo maelezo mengi kutoka vyanzo vingi vya vitabu na simulizi za wenyeji asilia wa jamii ya kabila la Wapare ambazo zimeelezea kuhusiana na maana halisi ya jina “Mkomazi” na asili yake. Ukweli halisi wa mambo ni ya kwamba jina hili limetokana na maneno mawili ambayo ni ‘Mko’ na ‘Mazi’ kutoka katika lugha ya kabila la Wapare yaliyounganishwa pamoja ambapo neno ‘Mko’ likimaanisha kijiko kidogo cha mti wa asili kilichotumika wakati wa kulia chakula na neno ‘Mazi’ ikimaanisha ni maji. Hii ilimaanisha ya kwamba kiasi cha maji kipatikanacho ndani ya eneo hili la hifadhi ni kiasi kidogo. Kihistoria jamii ya kabila la Wapare ni jamii ya Wabantu na chimbuko lao asilia limeanzia kusini mwa Taifa la Kenya katika safu ya Milima ya Taita ambayo ni mojawapo ya safu ya Milima ya Tao la Mashariki (Eastern Arc Mountains). Hifadhi hii ya Taifa ya Mkomazi kijiografia inapatikana mkoani Kilimanjaro pamoja na mkoani Tanga.

Ushauri kwa watalii raia wa Tanzania katika kujiandaa na kujipanga kimaandalizi na kikamilifu kwa safari utalii

IMG_5971

Iwe ni usafiri utalii wa binafsi au wa kukodi, ikumbukwe na ieleweke ya kwamba fedha zinahitajika kama mojawapo ya mambo muhimu ya kimsingi ya maandalizi na bajeti ya fedha hizi zinahitaji umakini mkubwa. Kikwazo na changamoto inayoukabiri utalii wa ndani ni usafiri pamoja na rasilimali fedha. Mtafikaje huko muendako hifadhini? Gharama za malazi na chakula je zimekaa vipi? Mtarudije na je safari utalii yenu ni ya siku ngapi? Je ni umbali kiasi gani mnakokwenda pamoja na kurudi? Hapa ni suala zima la mpango mkakati.

Hifadhi ya Taifa Mkomazi ilianzishwa na kupewa hadhi ya Hifadhi ya Taifa kutoka Pori la Akiba la Mkomazi – Umba na kutangazwa rasmi kupitia tangazo la Serikali Namba 27 la tarehe 14 Mwezi Machi mwaka wa 2008.

Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi ina ukubwa wa eneo lenye kuwa na kilometa za mraba 3,245. Hifadhi ya Taifa Mkomazi imetokana na Pori la Akiba la Mkomazi – Umba iliyoanzishwa toka mnamo mwaka wa 1951 wakati ambao eneo hili lilimegwa na kutengwa na Serikali ya kikoloni kutoka kwenye Pori Kuu Tengefu la Ruvu ambalo lilikuwa na eneo lenye kuwa na kilometa za mraba takribani 3,600 na kuwekwa chini ya Mamlaka ya Idara ya Wanyamapori.

Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi inafikika kwa njia ya usafiri wa barabara takribani umbali wa kilometa 120 kutoka Moshi Mjini mpaka wilayani Same Mkoani Kilimanjaro. Vilevile ni sawa na umbali wa kilometa 155 kutoka katika kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Kilimanjaro (KIA); ni sawa na umbali wa kilometa 200 kutoka Mkoani Arusha. Nairobi, nchini Kenya ni sawa na umbali wa takribani kilometa 480, wakati ambapo kutokea jijini Dares – Salaam ni sawa na umbali wa takribani kilometa 500. Kijiografia, Hifadhi ya Taifa Mkomazi inapatikana katika ukanda wa kaskazini mwa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, katika Mikoa ya Kilimanjaro (wilayani Mwanga na Same, takribani asilimia 61) pamoja na Tanga (wilayani Lushoto, Korogwe na Kilindi, takribani asilimia 39). Hifadhi ina umbo kama la Mstatili, ikiwa na urefu wa wastani wa kilometa 130 kutokea upande wa Mashariki kuelekea upande wa Magharibi na ina upana wa kilometa 41 kutokea upande wa Kaskazini kuelekea upande wa Kusini. Pia imenufaika kwa kuwa zaidi ya nusu ya urefu wake ikipakana kimipaka na Hifadhi ya Taifa ya Tsavo – Magharibi nchini Kenya kupitia mpaka wa kimataifa, ambapo wanyamapori hupata uhuru wa kuvuka kutoka upande mmoja kwenda upande mwingine wa mpaka huo.

Milima ya Upare Kusini na Kaskazini; maeneo ya wazi yenye kuwa na miti ya mapori na uoto wa nyasi; uoto wa misitu wa maeneo tambarare katika maeneo makame; uoto wa asili wa maeneno makame wenye kutawaliwa na uoto wa miti ya migunga na mbabara au mturimturi (Acacia - Commiphora). Kiujumla Hifadhi ya Taifa Mkomazi kawaida yake ni kame yenye kuwa na misimu miwili ya mvua ambapo msimu mrefu ni baina ya Mwezi Machi pamoja na Mwezi Mei na msimu mfupi kawaida ni kati ya Mwezi Oktoba pamoja na Mwezi Desemba. Wastani wa mvua kwa mwaka ni milimita kati ya 570 katika uwanda wa chini na milimita 1,910 kwenye uwanda wa juu. Vipimo vya joto ni nyuzi joto baina ya 18 pamoja na 29; Mwezi Julai na Mwezi Agosti ni miezi yenye kuwa na baridi. Uoto wa asili wa mimea aina ya ‘Acacia – Commiphora’ umegawanyika katika makundi mawili; misitu mikavu ya nyanda za juu iliyopo katika upande wa magharibi mwa Hifadhi pamoja na mbuga zenye kuwa na vichaka vidogo na nyasi katika uwanda wa chini wa Hifadhi. Upande wa kusini mwa Hifadhi ya Taifa Mkomazi ni Milima ya Tao la Mashariki (Eastern Arc Mountains) ya Upare na Usambara yenye kuwa na miamba mgandamizo.

Inaanzia katika kilele cha mlima Kinondu mita 1600 kutoka usawa wa bahari.

  1. Sehemu ya uoto wa asili wa jangwa la SAHEL unaowakilishwa na mimea ya miti aina ya MIGUNGA na MTURITURI (Acacia – Commiphora) ambapo katika Afrika Mashariki huishia katika Hifadhi ya Taifa Mkomazi nchini Tanzania.
  2.  Mandhari nzuri yenye kupendeza ya safu ya milima yenye kuwa na miinuko mipana pamoja na makorongo.
  3. Uwepo wa aina mbalimbali za viumbe hai ndege takribani zaidi ya spishi 450 ikihusisha kwa pamoja ndege wakazi (residents) na ndege wahamaji (migrants) kutokea katika mabara ya Ulaya na Asia kama European Roller.
  4. Uwepo wa viumbe hai wanaotambaa (reptiles) kama vile chatu, mijusi, pamoja na kenge.
  5. Upatikanaji wa aina mbalimbali za mammalia wadogo pamoja na wakubwa kama vile Kongoni, Duma, Twiga, Choroa, Swala Twiga, Pundamilia, Mbwa mwitu, Tandala wadogo, pamoja na mammalia wakubwa kama vile Tembo (Ndovu), Simba, Nyati
    (Mbogo), Chui na wengineo wengi
  6. Mandhari nzuri yenye kupendeza ya milima ya Upare.
  7. Idadi kubwa ya swala twiga, mandhari nzuri yenye kupendeza wa mlima Kilimanjaro na safu ya milima ya usambara magharibi, ndege wahamao, mapango katika miteremko ya milima ya Upare

Ni pamoja na utalii wa kuangalia wanyamapori katika nyakati za mchana kwa kutumia magari (Vehicle Game Viewing). Utalii wa matembezi ya miguu (masafa mafupi na masafa marefu). Utalii wa utazamaji viumbe hai ndege (bird watching). Utalii wa kuangalia wanyamapori sambamba na upigaji picha.

Tembo (Ndovu), Twiga, Swala twiga, Swala granti, Tandala wadogo, Kongoni, Mbogo (Nyati), Pundamlia, Ngiri, Tohe, Kuro, Swala pala, Pofu, Choroa, Digidigi, Mbweha masikio, Mbwa mwitu, Paka pori, na kadha wa kadharika. Hifadhi ya Taifa Mkomazi imerekodi kuwepo na zaidi ya spishi 450 za viumbe hai ndege mbalimbali kama vile Ndege Mbuni.

Hifadhi ya Taifa Mkomazi inaangukia katika ukanda wa uoto asilia wa maeneo makame unaofahamika kiutalamu kama (Somali – Maasai Arid Zone) ambapo uoto wa asili ya mimea wa miti ya migunga na mbabara / mturituri (Acacia - Commiphora) umetawala au kutamalaki. Vile vile maeneo wazi au uwanda mpana wenye kutawaliwa na uoto wa asili. Upatikanaji wa mvua katika maeneo haya ni mdogo sana na unaanzia milimita za mvua kwa mwaka (300 mpaka 700). Mazingira ya makazi ya eneo hili hayana tofauti na mazingira ya makazi ya hifadhi ya Taifa ya Tarangire pamoja na Hifadhi ya Taifa Serengeti. Uoto huu wa (Acacia – Commiphora) umegawanyika katika makundi mawili; misitu mikavu ya nyanda za juu iliyopo magharibi mwa Hifadhi na mbuga zenye kuwa na vichaka vidogo na nyasi katika uwanda wa chini wa Hifadhi.

Ni kuanzia Mwezi wa Juni mpaka Januari.

Ikumbukwe na ieleweke ya kwamba kwa raia Watanzania watalii wa ndani waliopo kwenye safari ya matembezi hifadhini wakajibebea vyakula vyao vya kujipikia wenyewe kama ikatokea ya kwamba mpango safari utalii wao unahusisha huduma ya kulala au kupiga kambi ndani ya Hifadhi.

Kama mtalala ndani hifadhini ni lazima kubeba mahema yenu kwa ajili ya kupiga kambi. Na kama hamtalala ndani hifadhini bila shaka ni vema utaratibu mwingineo ukaandaliwa ni sehemu gani ya malazi au kulala itakayotumika. Ndani ya Hifadhi ya Taifa Mkomazi kunapatikana huduma ya kambi ya kudumu, kambi maalumu na kambi ya jumuiya. Nje ya Hifadhi ya Taifa Mkomazi pia kunapatikana aina mbalimbali za huduma za Nyumba za kulala wageni {GUEST HOUSES), pamoja na HOTELI katika mji wa SAME (wilayani SAME).

Maandalizi ya usafiri, huduma za chakula, malazi au kulala, pamoja na huduma za mahitaji mengineyo ni nguzo bora na imara katika kufanikisha safari utalii yenu yenye kuwa na furaha na kumbukumbu isiyosahaurika. Tozo katika Hifadhi huhusisha mambo yafuatayo ya msingi kama vile; 1.Tozo ya uhifadhi/kiingilio (Mtu mzima, mtoto wa miaka 5 hadi 15, mtoto wa miaka 4 kushuka chini). 2. Tozo ya kupiga kambi maalumu (special campsites)/Mtu mzima (miaka 16 na zaidi), Mtoto (miaka 5 hadi 15), Mtoto (miaka 4 kushuka chini), kambi za kuhamahama. 3. Tozo za utalii wa matembezi ya miguu (kwa mtu kwa siku) umbali mfupi takribani saa 4 (Mtu mzima – miaka 16 na zaidi/ Mtoto – zaidi ya miaka 12). Umbali mrefu zaidi ya saa 4 (Mtu mzima miaka 16 na zaidi)/ Mtoto zaidi ya miaka 12). Tozo za uongozaji wageni watalii hifadhini wakiwa ndani ya gari au tozo za Askari wa wanyamapori katika matembezi ya miguu kwa kikundi kwa safari utalii. 4. Tozo za magari (uzito hadi kilogramu 2,000, 2,001 mpaka 3,000, 3,001 mpaka 7,000, 7,001 na kuendelea). Magari ya wazi yatalipiwa ada ya ziada ya asilimia 50 ya magari ya kawaida. Faini ya ajali au kuua mnyamapori pamoja na mwendo kasi kwa magari – aina zote za magari. 5. Tozo ya kupiga picha za matangazo ya biashara (hujumuisha ada ya kuingia pamoja na kupiga kambi hifadhini bila kujali utaifa wa mpiga picha. 6. Tozo za wanafunzi wanaosoma nchini Tanzania na ambao pia wanaotoka kwenye taasisi baada ya kuomba na kupata kibali kutoka kwa Kamishna Msaadizi wa Uhifadhi. 30 - 7. Tozo ya kutua Ndege za Tanzania na kibinafsi (kuanzia abiria watu 4, 5 mpaka 12, 13 hadi 20, pamoja na zaidi ya abiria watu 20). Kitu cha msingi cha kuzingatia ni ya kwamba Tozo hizi hazijumuishi Kodi ya Ongezeko ya Thamani (VAT – Asilimia 18). Tozo hizi zinaweza kubadilika, huwa halali kwa saa 24 na pia kwa kuingia mara moja tu). Jinsi ya ulipaji Tozo. Kwa kutumia Master Card, VISA (hii ni kwa wageni watalii wa ndani na wageni watalii wa nje). Vilevile ulipaji Tozo unaweza pia kutumia M – Pesa, Tigo Pesa na Airtel Money kwa raia Watanzania watalii wa ndani. Wageni wa nje wakazi (Expatriates) pia uhurusiwa kulipa Tozo kwa pesa za Kitanzania (Tshs).

Elimu na mafunzo ya huduma ya kwanza ni muhimu kuzifahamu. Katika vikundi vyetu vya watanzania watalii wa ndani tunaweza kuwa na timu maalumu kwa zoezi hilo. Sheria za uhifadhi na taratibu ni wajibu wa kila mtalii wa ndani na nje katika kuzitii na kuzitekeleza.

Mambo muhimu ya kufahamu na kujiuliza

Je safari utalii yenu ya matembezi hifadhini ina vifaa vyote muhimu vya kimatembezi hifadhini? Kanuni na taratibu za hifadhi ni muhimu sana kutekelezwa ili kuepuka matatizo ambayo si ya msingi kujitokeza kama vile faini.

Mkomazi-5

Vifaa vya kuchukua katika safari utalii hifadhini

Vifaa vyote muhimu katika safari utalii yenu ya matembezi hifadhini kama vile kamera kwa ajili ya kumbukumbu zenu ingawa leo hii simu janja zinafaa pia. Viona mbali (Binoculars) pamoja na vitabu vya hifadhi husika vya wanyamapori na ndege.

Huduma za mahitaji mengineyo

Mambo ya ziada ya mahitaji yanayojitokeza na upatikanaji wake katika sehemu husika. Hifadhi ya Taifa Mkomazi pia inatoa huduma na miundombinu mingine kwa mujibu ya uhitaji wa aina ya watalii na mahitaji yao wanayopendelea. Hii ni pamoja na uongozaji wageni watalii ndani ya hifadhi, utoaji maelezo kwa wageni watalii kuhusiana na rasilimali zipatikanazo hifadhini pamoja na sehemu za mapumziko ya kujipatia chakula (picnic sites)

Maelezo ya huduma za habari utalii wa ndani.

MAWASILIANO MENGINEYO MAKAO MAKUU (TANAPA)

+255 272508216

info@domestictourismsafaris.c  info@domestictourismsafaris.co.tz